Tafakari ya Dominika

MOYONI UMEJAZA NINI?



Jumapili ya 22 ya Mwaka B



“…Kwa maana kutoka ndani ya watu, kutoka mioyo yao, yanatoka mawazo mabaya; uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, choyo, ukorofi, hila, ufisadi, wivu, matusi, kiburi, upumbavu.Maovu hayo yote yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi” (Marko 7: 15-23)




Lililo moyoni ulimi huiba. Ukiongea neno zuri ulimi utakuwa umeliiba toka moyoni. Ukiongea neno baya ulimi unaliiba toka moyoni. Swali moyoni umejaza nini? Moyo ni makao ya mawazo mazuri na mawazo mabaya. Ni makao ya hisia, hamu, huba na chuki. Chunga sana moyoni umejaza nini? Kuna mtu alikuwa anamkimbiza adui yake ili apate kumua wakati anamkibiza saa ya kusali ikatimia, akapiga magoti kusali haraka haraka akainuka na kuanza kumkimbiza adui tena amufute kwenye uso wa dunia. Ina maana moyoni amejaza hasira, mawazo ya kuua na si mawazo juu ya Mungu. Moyo uko mbali na Mungu. Hilo ndilo jambo lililomsumbua Yesu dhidi ya wafarisayo na alisema, “Watu hawa huniheshimu kwa midomo, lakini mioyo yao iko mbali” (Marko 7:7).



Mwizi alulizwa na hakimu kwa nini ulirudi mara ya pili kuiba katika duka. Mtu huyo alijibu kuwa aliona maneno yameandikwa karibu tena. Mwizi alikuwa moyoni amejaza visingizio na mawazo ya kuiba. Moyoni umejaza nini? “Hakuna kitu kinachomwingia mtu kutoka nje kinachoweza kumnajisi; bali vitu vimtokavyo mtu vyamtia unajisi….Kwa maana kutoka ndani ya watu, kutoka mioyo yao, yanatoka mawazo mabaya; uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, choyo, ukorofi, hila, ufisadi, wivu, matusi, kiburi, upumbavu.Maovu hayo yote yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi” (Marko 7: 15-23)



Kwenye orodha anaanza na mawazo mabaya. Moyoni hutoka matashi mabaya au mawazo mabaya. Tendo lolote linaloonekana linatanguliwa na chaguo la moyo. Matendo mabaya hutokana na mawazo mabaya. Kiongozi wa kidini wa huko Mashariki Dalai Lama anasema kuwa unapokutana na mtu ambaye labda ni adui yako fikiria au jenga picha kuwa anakusifia au anakupa zawadi mara hisia zako kumwelekea mtu huyo zitabadilika. Mawazo mazuri yanazaa hisia nzuri na mawazo mabaya yanazaa hisia mbaya. Ndugu wawili walienda kwa Mchungaji ili awasaidie kusuluhisha ugomvi wa siku nyingi. Mchungaji aliwapatanisha ndugu hao wawili na wakapeana mikono ya amani. Kabla ya ndugu hao hawajaondoka mchungaji aliwaambia kila mmoja amtakie mwenzake jambo zuri. Ndugu mmoja alimgeukia kaka yake na kumwambia, “Mimi nakutakia yote unayonitakia.” Yule ndugu wa pili alianza kulalamika akamwambia mchungaji, ‘Anaanzisha ugomvi tena.” Mchungaji akauliza kwa mshangao, “Kwani wewe haumtakii mazuri?” Mtume Paulo anatuasa, “Ndugu, yaliyo kweli, matukufu, adili, yaliyo matakatifu, ya kupendeza na ya sifa njema, yote yanayohusiana na ukamilifu, tena masifu, hayo yafikirieni hasa” (Wafilipi 4:8). Mawazo mazuri lazima yawe na sifa nane zilizotajwa kwenye somo hilo.





Moyoni hutoka uchoyo. Watu wenye uchoyo hupoteza zaidi kuliko wanavyopata. Hauwezi kuwa na choyo na ukawa na furaha wakati huo huo. Mawazo ya uchoyo hayana sifa za mawazo mazuri. Uchoyo hauna sifa ya ukweli, utukufu, adili, utakatifu, kupendeza, sifa njema, ukamilifu au ubora. Kilicho na sifa hizo ni ukarimu. Uchoyo una sura tatu: kupenda vitu, kupenda sifa, na kupenda anasa. Kutokana na mambo matatu tunapata tamaa ya mali, majivuno na tamaa ya mwili. Kuna watoto wawili waliokuwa wanakula chakula. Palibaki vipande viwili vya nyama ya kuku. Kimoja kipande kikubwa na kingine kipande kidogo. Wakaanza kugombania kipande kikubwa nani akichukue. Mama yao akawaambia kama mmoja wenu angekuwa Yesu, angesema, “Mimi nachukua kipande kidogo wewe chukua kipande kikubwa.” Mtoto mkubwa akamwambia mdogo wake, “Basi wewe kuwa Yesu na uniambie maneno hayo.” Mtoto mkubwa hakuwa tayari kuwa kama Yesu.



Moyoni hutoka uongo. Mwalimu alimuuliza mwanafunzi aliyeitwa Frank, “kwa nini umechelewa, Frank?” Frank alijibu, “Kwa sababu ya alama.” Mwalimu aliuliza, “Alama gani?” Frank alijibu, “Ile isemayo, “Kuna Shule Mbele, Nenda Polepole.” Alama hiyo ni kwa ajili ya gari au pikipiki na si kwa ajili ya watembeao kwa miguu. Hapo kuna uongo.



Moyoni hutoka mawazo ya wizi. Katika lugha ya Kigriki mojawapo ya lugha zilizotumiwa kuandika biblia kuna maneno mawili yanayomaanisha mwizi. Neno la kwanza ni mnyang’anyi kama Baraba. “Baraba alikuwa mnyang’anyi” (Yohana 18: 40). Pili mdokozi kama Yuda Iskarioti. Yuda Iskarioti alipoona mwanamke anampaka manukato Yesu alisema, “Mbona manukato hayo hayakuuzwa kwa dinari mia tatu na kuwapa maskini, ila kwa sababu alikuwa mwizi, aliutunza mfuko wa fedha na alikuwa anajihudumia kwa fedha hizo” (Yohane 12:6). Polisi alimuuliza mwizi hauoni aibu kila mara unapoweka mkono wako kwenye mfuko wa mtu kumwibia. Mwizi alisema naona aibu nisipokuta kitu chochote. Huyo ana mawazo ya wizi. Ana mawazo ya udokozi. Amri ya kumi inatukumbusha usitamani mali ya mtu mwingine.



Moyoni hutoka upumbavu. Mawazo ya kipumbavu hayana maana kabisa. Ni ukweli uliogeuzwa. Ni ukweli ulio shaghalabagala. Kuna methali ya Kiganda isemayo, “Ni mbwa mpumbavu tu ambwekeaye tembo.” Ni kama mbwa afukuzaye gari akilifikia gari atafanya nini. Methali ya kiafrika inasema yote. Ni upumbavu na si ujasiri kupanda mti wa miiba. Katika upumbavu mtu ujihumiza. Siku moja panya alisimama karibu na mto akimuita kiboko, kiboko alipotokeza akauliza kwa nini anaitwa. Panya akasema alitaka kuona kama ana nguo zake za kuogelea. Nguo ambayo inaweza kumkaa panya haiwezi kumkaa kiboko. Huo ni upumbavu. Hayati Abrahamu Lincoln aliyewahi kuwa Rais wa Amerika alituachia maneno ya busara. “Ni vuzuri zaidi kukaa kimya na kufikiriwa wewe ni mpumbavu kuliko kusema na kuondoa mashaka yote.” Ifanye sala ya mfalme Daudi iwe sala yako: “Uniumbie moyo safi ee Mungu” (Zaburi 51: 12).



Moyoni hutoka mawazo ya uzinzi. Uzinzi ni kukosa uaminifu wa ndoa (KKK 2380). Ni kuvunja mkataba wa ndoa. Ni ukosefu wa haki. Ni kuharibu taasisi ya ndoa. Kuna maneno kwenye kanga za wakina mama yasemayo: “Mtamaliza bucha bure, nyama ni ile ile.” Biblia yasema, “Mke wako ni kama kisima cha maji safi; kunywa maji ya kisima chako mwenyewe” (Methali 5:15). Visima ningine hujui nani kapitia, hujui kama maji ni safi na salama. “Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake” (Mt 5:28). Kanisa Katoliki lafundisha: “Pambano dhidi ya tama za mwili hufanyika kwa kutakasa moyo na kushika kiasi: “Mwe wanyenyekevu na wanyofu na mtakuwa kama watoto wadogo wasiojua ovu linaloharibu uhai wa mtu” (KKK 2517).



Moyoni hutoka mauaji. Chanzo cha mauaji ni moyo. Moyo ni kiti cha utu adili, lakini moyo waweza kuwa kiti cha mawazo ya mauaji. Katika nchi fulani kuna aliyeua wazazi wake. Alihukumiwa kifungo cha maisha. Alipoombwa kujitetea alisema anaomba apunguziwe kifungo yeye ni yatima. Mauaji ni mauaji. Hakuna kisingizio. Chuki ni kama mauaji. “Yeye asiyependa akaa katika mauti. Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mwajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ndani yake” (1 Yoh 3:14-15). Mungu pekee ni Bwana wa uzima. Kuna Padre Vincent McNabb alikuwa anahubiri mahubiri yake yalimkasirisha mama mmoja. Akasimama na kusema wewe padre ungekuwa mme wangu ningekuwekea sumu kwenye chain aye Padre akasema, “Kama ungekuwa mke wangu jinsi ulivyo. Ningekunywa hiyo sumu.” Mwanamke huyo alikuwa na chuki.



Moyoni hutoka matusi. Tusi ni neno chafu. Ni suto. Ni tukano. Kutusi ni kutukana. Ni kusuta mtu kwa maneno machafu. Matusi hayaelezei mtu jinsi alivyo. Ni tusi kumuita mtu mwungwana mhuni. Ni tusi mtu aliyeumbwa katika sura na mfano wa Mungu kumwambia, uso wake unafafana na karatasi yenye majibu ambayo siyo sahihi. Sio heshima kutusi watu. “Anayemdhihaki maskini anamtukana Muumba wake” (Methali 17: 5) Maana mtu ameumbwa kwa mfano na sura ya Mungu. Sio uungwana kutusi watu. Mungu haumbi takataka. Matusi kwa kawaida hayaunganishi watu bali yanagawanya watu. Matusi yanajenga kuta badala ya daraja. Matusi mengine yanaweza kumgeuka anayetukana.



Wakati wa kampeni ya uchaguzi kati ya Douglas Stephen Arnold (1813 – 1861) na Abraham Lincoln (1809 – 1865) Rais wa kumi na sita wa Amerika. Douglas aliwaambia watu kuwa wasimchague Abraham Lincoln kwa vile alikuwa anafanya biashara ya kuuza pombe kali. Labda Douglas alitaka kuwaambia watu kuwa Abraham ni mlevi ingawa katika maisha anayehuza pombe haina maana ni mlevi. Naye Abrahamu Lincoln katika kumjibu Douglas alisema kuwa, mteja wake mkubwa alikuwa Douglas nay eye alisha acha biashara ya kuuza pombe lakini Douglas achaacha kuwa mteja kwa wenye baa. Neno alilolisema Douglas liligeuka na kuwa bumerengi yaani hoja au pendekezo ambalo humrudia mtoaji na kumdhuru. Matusi mengine yanakuwa bumerengi.





Kutukana mtu ni kujiletea laana na mikosi katika maisha. Mtu anayetukanwa ameeumbwa kwa sura na mfano wa mwenyezi Mungu. Daudi katika biblia aliposikia kwamba Nabali amekufa, alisema, “Atukuzwe Mwenyezi Mungu ambaye amemlipizia kisasai Nabali kwa kunitukana, naye Mwenyezi Mungu ameniepusha mimi mtumishi wake kutenda maovu. Mwenyezi Mungu amempatiliza Nabali kwa uovu wake.” ( 1 Samweli 25: 39) Tusi la Nabali bila shaka lilikuwa zito. Kipimo cha uzito wa matusi kinategemea mambo mengi kama cheo cha yule aliyetukanwa, umri wa yule anayetukana, aina ya tusi na athari za tusi hilo, mazingira ya matusi hayo, lengo la mtukanaji. Katika visa mbalimbali hapa Afrika pamekuwepo na visa vya watu kuwafikisha wengine mahakamani kwa kuwaharibia jina kwa njia ya matusi ambayo yamejaa kashfa na uzushi. “Ukimtukana rafiki hutavunja urafiki.” (Sira 22:20)





Moyoni hutoka wivu. Kuna njia nyingi kuelekea nchi ya chuki lakini njia fupi kuliko zote ni husuda au wivu. “Wivu huwapiga risasi wengine na kujihumiza wenyewe.” Ni methali toka Sweeden. “Ni mpumbavu tu ambaye hunywa maji katika kisima cha wivu.” Ni methali toka Niger. “Kama wivu hungekuwa unawaka tusingehitaji kuni.” Ni methali ya Yugoslavia. Methali hii inamaanisha wivu hauna faida. Wivu ni kijicho, ni husuda. Wakati mwingine mtu akiwa na maisha mazuri jamaa na marafiki zake huwa na wivu au husuda juu yake. Kumwonea mtu wivu ni kukubali kuwa wewe ni dhaifu mbele yake. Mwenye wivu hawezi kamwe kumsifia mtu aliyefanya vizuri. Wivu au kijicho ni kutopendelea kuona usitawi wa mtu mwingine. Haifai kuwa na kijicho na mwenzako; Mungu aliyempa yeye ndiye atakayekupa na wewe. Wivu ni huzuni anayokuwa nayo mtu sababu mwenzake kapiga hatua maishani. Husuda ni uchungu kwa kuona mali za mwingine na hamu isiyo na kiasi ya kutamani kuzipata kwa ajili yake. Ni kasoro kubwa.





Kati ya wapendanao kuna wivu ambao unasaidia kujenga na wala si kubomoa. Mwanamke aliyeitwa Anna alitaka kukomesha tabia ya mme wake Solomoni ya kurudi nyumbani usiku wa manane. Bwana Solomoni alipobisha mlango na kusema: “Hodi, nifungulie!” Mke wake aliuliza, “Je, ni wewe Isaka!” Mme wake aliona wivu na kufikiria kuwa akitoka na kuchelewa kurudi anakuja nyumbani mwanaume aitwaye Isaka. Hakuchelewa tena nyumbani alikuwa akiingia nyumbani kabla hata ya kuku kuingia kwenye mabanda jioni.



HITIMISHO

“Ni moyo unaompelekea mtu mbinguni au motoni.” Ni methali ya Kiafrika. Mungu hatazami sura ya nje anatazama yaliyomo moyoni. Mwenyezi Mungu alimkataa Eliabu hasiwe mfalme wa Israeli kwa vile Mungu hatazami sura ya nje, hatafuti warembo wa sura bali warembo wa moyo. Tunasoma katika Biblia, “Usiangalie sura yake na urefu wa kimo chake. Mimi nimemkataa kwani siangalii mambo kama wanavyoangalia binadamu wenye kufa. Binadamu huangalia uzuri wa nje, lakini mimi naangalia moyoni” ( 1 Samueli 16: 7).



Maisha yako ni kama kitabu. Kichwa cha kitabu ni jina lako; Dibaji ni kuingia kwako duniani. Kurasa ni yale ambayo unajaza kila siku: mazuri, mabaya, maneno yako, furaha, majonzi. Mawazo yako yanaandikwa kila siku. Siku moja neno “Mwisho” litaandikwa katika kitabu chako. Kitabu chako kiwe rekodi ya malengo mazuri, kazi nzuri. Biblia yatuasa, “Angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima, bali kama watu wenye hekima.” Ili kuzaa matunda mema moyoni ujaze mawazo mazuri.

No comments:

Post a Comment